Sunday, April 7, 2013

Utangulizi wa Lugha na Isimu 1KSW 101: UTANGULIZI WA LUGHA NA ISIMU

*        Muhadhara wa kwanza

MAANA YA LUGHA

1.0.            Lugha ni nini?

Mtu anapouliza swali hili (Lugha ni nini?) inaweza kuonekana kana kwamba ni swali la kijinga. Labda kwa sababu huwa hatupendi kutilia maanani katika vitu ambavyo tunadhani ni vya kawaida. Kwa bahati mambo hayapo kama tunavyoweza kuyaona au kuyatafakari. Kwa maana hiyo basi, hata swali la kwamba “lugha ni nini?” siyo rahisi na wala siyo la kawaida kama ambavyo tunaweza kulichukulia. Kwa maelezo hayo tunaweza kufasili dhana ya lugha kwa mitazamo miwili: Mtazamo finyu (narrow conception) na Mtazamo mpana (Broad conception).

1.1.            Mtazamo Finyu:

                                i.            Lugha ni chombo cha mawasiliano
Kuitazama lugha kama tu chombo cha mawasiliano kunawezesha ufahamu wa kawaida. Kwa maana hiyo, bado kuna taarifa muhimu zinakosekana katika fasili na hii inatupatia mapungufu ya fuatayo: kwanza, kueleza lugha kama chombo cha mawasiliano ni kueleza kazi ya lugha na sio lugha yenyewe. Pili, kama mtu atapiga ngoma ili kuwaita watu na watu wakaja basi milio ya ngoma itakuwa ni lugha. Na kwamaana hiyo kila kitakacho wawezesha watu kuwasiliana kitakuwa ni lugha. Kama lugha ni chombo tu cha mawasiliano, maana yake hakuna tofauti yoyote kati ya kuzungumza na milio mbali mbali kama honi ya gari, filimbi ya refa uwanjani, au kengere ya kanisani au hata sauti inayotokana na kugonga mlango wakati mtu anabisha hodi. Hivyo jambo hili sio la kweli na linatupeleka mbali zaidi na kutufanya tuanze kuitazama fasili ya lugha kwa mtazamo mwingine zaidi – mtazamo mpana.

1.2.            Mtazamo Mpana.

Katika mtazamo huu kunawanaisimu wengi ambao wamejaribu kutoa fasili zao mbali mbali. Baadhi ya fasili hizo ni kama zifuatazo:
i.                    Todd (1987) anasema lugha ni mfumo wa ishara ambazo kwazo watu huwasiliana.
ii.                  Kamusi ya Isimu na lugha (1990) inaeleza kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.”
iii.                Cook,1969:12 anaeleza kuwa lugha  ni mfumo wa sauti nasibu na ishara za kisarufi ambazo kwazo watu wa jamii Fulani ya lugha huwasiliana na kupokezana utamafuni wao.
iv.                Bloch and Trager (1942): “A language is a system of arbitrary vocal symbols by means of which a social gorup co-operates”.
[“Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo kwazo makundi ya kijamii hushirikiana”]

v.                  Noam Chomsky(1957): “Language is a set of finite number sentences, each finite in lingth and constructed out of a finite set of elements”
[Lugha ni seti ya idadi ya sentensi zinazojitosheleza, kila idadi inajitosheleza kwa urefu na hujengwa kutokana na seti za elementi zinazo jitosheleza”.]
vi.                 Michael Halliday (2003): “A language is a system of meaning- a semiotic system”
[“Lugha ni mfumo wa maana – yaani mfumo wa ishara (semiotic system)”]
vii.              Muharrem Ergin(1990):Language is a natural means to enable communication among people, a living entity that it has its own peculiar laws, by means of which alone can it develop, a system of contracts whose foundation was laid in times unknown, and a social institution interwoven with sounds”.
[“Lugha ni njia ya asili ya kuwezesha mawasiliano miongoni mwa watu, ni chombo hai yaani chenye sheria zake za pekee ambazo kwazo peke yake hujijenga, ni mfumo wa makubaliano ambao misingi yake iliwekwa katika wakati usiojulikana, na ni taasisi ya kijamii ambayo imechangamana na sauti.]
viii.            Language: The system of arbitrary vocal symbols we use to encode our experience of the world”
[Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo tunazitumia kusimba uelewa na uzoefu wetu wa ulimwengu.]

ix.                Nae Sapir (1921:7) anasema: “Language is a purely human and non-instinctive method of communicating ideas, emotions and desires by means of voluntarily produced symbols.”
[Lugha ni njia ya mawasiliano ambayo ni maalumu kwa mwanadamu na isiyo silika ambayo hutumiwa kuwasilisha mawazo, hisia na matakwa kwa kutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiyali].

x.                  Mario Pei & Frank Gaynor (1954) Kamusi ya Isimu (A Dictionary of Linguistics) anasema: Language is a system of communication by sound, i.e., through the organs of speech and hearing, among human beings of a certain group or community, using vocal symbols possessing arbitrary conventional meanings.
[Lugha ni mfumo wa mawasiliano kwa njia ya sauti, yaani, kwakutumia alasauti na kusikia, miongoni mwa binadamu wa kundi fulani au jumuiya kwa kutumia ishara-sauti ambazo maana zake hueleweka kwa unasibu tu.

2.0.            Tathmini ya Fasili za Lugha

Ukichunguza fasili hizi na nyingine nyingi ambazo hazijatolewa hapa utagundua kuwa swali letu tuliloliuliza hapo mwanzo yaai “Lugha ni nini?” sio swali la kijinga wala sio swali rahisi kulijibu. Hivyo basi, kutokana na fasili hizo tunaweza kusema kuna maana mbali mbali za lugha kulingana na mzingira, mazoea, taaluma na hata mahala mtu alipobobea kitaaluma. Lakini, pamoja na tofauti hizi mbali mbali zinazojitokeza, tunaona kuna mambo kadhaa ya msingi ambayo takribani wataalamu wote wanayagusia wanapofasili dhana ya ‘lugha’. Mambo hayo ni kama yafuatayo: Lugha ni mfumo, Lugha ni mfumo wa sauti nasibu, Lugha ni maalumu kwa binadamu, Lugha ni mfumo wa ishara, Lugha hutumia sauti, Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano. Kimsingi mambo haya ndiyo yanayogusiwa katika fasili hizi. Lakini ikumbukwe kuwa, sio kila fasili zilizotajwa hapo juu zinajumuisha vipengele vyote hivi. La hasha! Fasili moja inaweza ikawa inakipengele kimoja wapo au viwili kati ya hivi. Kila kimoja kinaelezewa hapa chini kama ifuatavyo.

2.1.            Lugha ni mfumo

Ishara zinazotumiwa katika lugha zinampangilio wenye kutawaliwa na sheria na unaruwaza zinazotambulika na watumiaji wa lugha hiyo. Kila lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya.
Katika muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazidhibiti mfuatano wa kila kipashio. Kuna kanuni zinazo dhibiti mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi. Hivyo basi, mtu hawezi kuunganisha tu sentensi kwa matakwa yake bila kujali kanuni hizi, akifanya hivyo atasababisha kutokea kwa kitu ambacho siyo lugha na wala hakikubaliki katika lugha. Kwa maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa basi kuna kuwa hakuna utimilifu wa lugha husika. Lugha inaonesha utaratibu katika mahusiano ya viunzi vya lugha. Sheria hizi zinazotawala mpangilio wa viunzi vya lugha hiyo ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana.

2.2.            Lugha ni mfumo wa sauti nasibu (Unasibu katika lugha ya mwanadamu)

Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno (mathalani kiti) na kitu chenyewe tunachotumia kukalia (maana na kilejelewa). Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa.
Tazama mchoro ufuatao:


Katika picha inayoonekana hapo juu kuna neno ‘mti’ na mmea wenyewe ambao umebatizwa jina hilo. Katika hali halisi hakuna watu waliokaa nakusema kuanzia leo huu utaitwa mti. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya neno “MTI” an umbo linalomaanishwa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutokana na lugha na lugha. Hii ndiyo maana Waingereza wataita tree, Wahehe wataita mubiki, Wasukuma wataita mpiki n.k. Ukweli kwamba hakuna uhusiano wa asili kati ya umbo la neno na maana ambazo umbo hilo linapewa ndiyo sababu inayofanya kuwe na namnatofauti ya kuuelezea ulimwengu. Ferdinand de Saussure katika kile alichokiita ishara za kiisimu anabainisha sawia mbili za mahusiano haya; kwanza ni “signifie” ambacho ni kiashiria yaani umbo la kifonolojia (kutamkwa) au kiothografia (kuandikwa) na ambalo huwakilisha dhana Fulani. Kitu cha pili ni “significant” ambacho ni kiashiriwa ambacho ni kitu chenyewe kilicho katika ulimwengu halisi wa vitu na dhana. Hivyo basi, uhusiano kati ya kiashiria na kiashiriwa ndio unlio wa unasibu.

2.3.            Lugha ni maalumu kwa mwanadamu.

Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu anauwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa Fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanawea kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu anauwezo wa kujifunza lugha mbali mbali na kutumia katika mazingira yake na sio wanyama. Kwa mfano, ukimtoa mbwa Tanzania na kumpeleka Japani, atatoa sauti ile ile sawa na mbwa wa Japani kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.

2.4.            Lugha ni mfumo wa ishara

Uishara wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa / huhusishwa na vitu, matendo, mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano. Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilisha.

2.5.            Lugha hutumia sauti

Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Tafiti zinathibitisha kuwa mfumo wa maandishi umekuja baadaye sana katika maendeleo ya binadamu na kwamba hutumika tu kuwasilisha yale yanayosemwa kwa kutumia kinywa cha mzungumzaji. Vile vile, ukweli kwamba binadamu anapozaliwa huanza kujua lugha ya mahala anapokua na kuishi kabla ya kufahamu kuandika, unatuthibitishia kuwa kiunzi (msingi) cha lugha ni sauti.
Kwa ujumla, kuna sababu kuu tano zinazotuwezesha kukubaliana kuwa msingi wa lugha ni sauti za kutamkwa.
i.        Mtoto hujifunza kuzungumza kablra hajajifunza kusoma na kuandika
ii.      Mtoto hujifunza lugha moja kwamoja bila kufikiri kadiri anavyokuwa.
iii.    Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
iv.    Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
v.      Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika
vi.    Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti z lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu, haya ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawa sawa kwakutumia maandishi (Habwe na Karanja, 2003).

2.6.            Lugha ni kwaajili ya mawasiliano

Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.

2.7.            Fasili ya jumla

Hivyo basi, baada ya kuchunguza fasili hizo za lugha na vipengele vinavyojibainisha kwenye kila fasili mojawapo, tunaweza kusema kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kilasiku kueleza hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.

3.0.            Tabia za lugha ya binadamu ainazoitofautisha na aina nyingine za mawasiliano

Tumekwisha elezwa hapo awali kuwa lugha ni maalumu kwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe yeyote ambaye si mwanadamu mwenye uwezo wa kujua, kujifunza na kutumia lugha zaidi ya binadamu. Jambo hili linatupelekea kuzitathmini sifa au tabia za lugha ya mwanadamu. Kimsingi sifa/tabia hizi ndizo zinazoitofautisha lugha ya mwanadamu na aina nyingine za mawasiliano zitumiwazo na wanyama.

3.1.            Unasibu

Kama tulivyokwisha eleza mwanzo, unasibu wa lugha ya ninadamu unaangaliwa katika mambo yafuatayo:
i.                    Binadamu hazaliwi na lugha, anakutananayo kwa unasibu tu
ii.                  Hakuna uhusiano wa moja kwa moja au wa asili kati ya kitaja (neno kama umbo la kiisimu) na kitajwa (kitu au umbo linalomaanishwa au maana). Uhusiano wake niwa unasibu na unatokana na makubaliano ya watumia lugha.
iii.                Hata makubaliano haya ya kwamba kitu kiitwe au dhana fulani iitwe na kuelezwa kwa namna fulani ni ya nasibu tu. Hapa tunamaanisha kwamba hakuna mkutano au kikao ambacho binadamu amewahi kukaa akasema mathalani neno “chuki” limaanishe hali ya kuto kumpenda mtu au neno “upendo” limaanishe hali ya kuonesha huba kwa mtu.
iv.                Kila jamiilugha ina namna yake ya kuufasili na kuuelezea ulimwengu kwa lugha yake ambayo inatofautiana na jamiilugha nyingine.

3.2.            Uzalikaji au Ubunifu

Uzalikaji katika lugha ya binadamu unajidhihirisha katika mambo yafuatayo:
i.                    Uwezo wa mwanadamu kubuni na kuunganisha maneno na miundo mbali mbali ya tungo bila kikomo.
ii.                  Uwezo wa mwanadamu kutunga na kuzielewa tungo mbali mbali ikiwa ni pamoja na zile ambazo hajawahi kuzisikia wala kuzitunga.
iii.                Uwezo wa mwanadamu kuelewa tungo zilizotungwa na watu wengine na kufahamu maana ya kisemantiki na ile ya kipragmatiki.
iv.                Uwezo wa mwanadamu kuzielewa tungo sahihi na zile zisizo sahihi
Hivyo uwezo huu unatofautiana na aina nyingine ya mawasiliano inayotumiwa na wanyama wengine, kwamfano, “nyenje ni myama mwenye milio au ishara nne za kuchagua ili awasiliane, tumbili ana miito sita tu. Hivyo wanyama wote hawa wanaidadi isiyobadilika ya milio na sauti au ishara na hawana uwezo wa kubuni namna nyingine ya kuwasiliana au kubuni milio mingine ya kuwasiliana.
3.3.            Uambukizaji wa utamaduni
Lugha ya mwanadamu inauwezo wa kuambukiza utamaduni kutoka katika kizazi kimoja kwenda kizazi kingine au kutoka katika jamiilugha moja kwenda katika jamiilugha nyingine. Ieleweke kuwa, uwezo huu wa kuambukiza maarifa ya lugha hufanyika kwa njia ya kusoma au kujifunza na sio kurithi. Kwa mfano, mtu anaweza kurithi maumbile kutoka kwa wazazi wake, mathalani aina ya nywele, aina ya macho, lakini mtu hawezi kurithi lugha. Lugha inamfikia kwa kuambukizwa katika jamiilugha anayokulia. Yatupasa tukumbuke kuwa, ingawa mwanadamu anazaliwa na uleuwezo (kitengo cha lugha) wa kujifunza lugha “Language Acquisition Device” kama anavyoeleza mwanaisimu Noam Chomsky, lakini hazaliwi na lugha. Hii ndiyo sababu mwanadamu anaweza kujifunza lugha yoyote ile na kwa wakati wowote maadamu yupo katika mazingira na hali ya kawaida na saidizi.

3.4.            Uwili (utamkaji pamwe)

Lugha ya mwanadamu imepangwa katika viwango viwili ambavyo vinashirikiana na kukamilishana. Kiwango cha kwanza ni kile kiwango cha utamkaji wa sauti au utoaji wa sauti kama; /n/, /m/, /g/, /t/, /k/, /a/, /e/, /o/ kwa kutumia alasauti mbali mbali. Sauti hizi zikisimama peke yake hazina maana yoyote, ni kama milio tu kama kupiga chafya, au kekele zinazotokana na kuburuza meza kwenye sakafu au kelele za injini ya piki piki. Sauti hizi zinapounganishwa (kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za lugha husika) tunapata maneno yenye maana ambapo tunapata kiwango kingine cha pili cha maana. Sifa ya uwili inadhiririsha sifa ya uwekevu katika lugha ya mwanadamu kwani kwa kutumia sauti hizi chache mzungumza lugha anaweza kutoa au kuzungumza sentensi nyingi au tungo nyingi na zenye maana tofauti tofauti bila kikomo.
Suala jingine la msingi ni kwamba, tunaposema kuwa lugha imegawanyika katika viwango viwili, kiwango cha sauti na kiwango cha maana haimaanishi kwamba binadamu anatumia viwango hivi kiupeke peke. Hata sikumoja mwanadamu hasemi kwamba sasa naanza kutamka sauti, mathalani, baba halafu ndiyo niweke maana yake. La hasha! Binadamu hutamka kwa maramoja sauti pamoja na maana vikiwa vimebebana ndani kwa ndani (hutamka sauti pamwe na maana). Yaani, wakati anatamka sauti na kuziunganisha ndiyo wakati anaambatanisha na maana ndani yake. Hii ndiyo sifa ua uwili katika lugha ya mwanadamu.

3.5.            Uhamisho au Urejelezi

Uhamisho ni sifa ya lugha ya mwanadamu inayomaanisha kwamba lugha ya mwanadamu inaweza kutumika katika kuzungumzia au kurejelea kitu ambacho hakipo katika upeo wa macho ya mzungumzaji kiwakati na kimazingira. Tofauti na mawasiliano ya wanyama, binadamu anaweza kuzungumza juu ya matukio yaliyopita, matukio yajayo, na hata yale anayoyatarajia kufanya kwa kutumia lugha. Kwa mfano, myana kama ng’ombe hawezi kuelezea kwa njia yake ya mawasiliano, aina ya chakula alichokula jana, au anachotamani kula, au anachotarajia kula, au kwa nini jana alikwenda kunywa maji, au hata kujua sababu ya kuumia. Lakini mambo haya binadamu anayaweza kwa kutumia lugha yale ya asili. Hii ndiyo sifa inayoitwa uhamisho au urejelezi (displacement).

3.6.            Uwezo wa kubadilishana taarifa/Ubadilishanaji taarifa

Sifa hii inamaanisha kuwa binadamu wenyewe kama watumia lugha wanauwezo wa kubadilishana taarifa. Kila mmoja wao anaweza kuwa mtumaji au mpokeaji wa taarifa kwa kutumia lugha.

3.7.            Upeke

Lugha hundwa na viunzi vidogo vidogo ambavyo ni peke peke na haipo katika mfululizo. Kila kipashio kinachotumika kuunda tungo za lugha kipo peke peke na kinaweza kuunganishwa na vingine kupata muundo wa juu mkubwa zaidi. Hivyo, lugha inawezwa kugawanywa tena kwa kukusayna vipashio hivyo kuunda tungo kubwa zaidi.

4.0.            Asili ya Lugha

Hakuna maafikiano kati ya wanaisimu juu ya wapi, lini, namna gani na nani hasa alianzisha lugha. Hii inatokana na ukweli kwamba binadamu alianza kuishi tangu kale wakati ambapo hata hivyo bado hauja julikana. Suala ambalo lina uhakika ni kuwa lugha inatumiwa na mwanadamu na kila jamii ina lugha yake. Hata hivyo kuna nadharia mbali mbali zinazoeleza chanzo na asili ya lugha. Baadhi ya nadharia hizo ni kama zifuatazo:

4.1.            Nadharia ya UUngu/mtazamo wa kidini

Msingi wa nadharia hii ni kwamba lugha iliumbwa na Mungu na akapewa mwanadamu kwa nguvu za Mwenyezi Mungu. Nadharia hii inaeleza kuwa, haja ya Mungu kuwasiliana na kiumbe wake Binadamu ndiyo iliyomfanya aumbe lugha. Inaaminika kuwa Mungu ndiye alikuwa wakwanza kutumia lugha, aliumba ulimwengu kwa kutumia neno, na kwa neno kila kitu akiwemo mwanadamu likifanyika. Inaaminika kuwa lugha zote zilitokana na lugha moja iliyoumbwa na Mungu. Hata hivyo kuna visasili mbali mbali vinavyoeleza asili ya lugha katika nadharia ya Uungu. Kwanza ni, pale Mungu alipompa Adamu uwezo wa kuzungumza kwa kuwatajia majina wanyama wote na pale ndipo lugha ilipoanza (Mwanzo 2:19).
Nadhari hii ya uungu pia huchagizwa na kisasili kingine cha Wamisri, Wababiloni, na Wahindi. Kwa mujibu wa kisasili cha Wababiloni, inasemekana hapo kale Mfalme wa Babeli aliamuru kujenga mnara mrefu ulioitwa Mnara wa Babeli ili kumfikia Mungu. Kwa lengo hilo Mungu alikasirishwa sana akaamua kuwachanganya lugha wajenzi wa mnara huo hivyo wakashindwa kuelewana na hatimaye azma yao ikasitishwa. Kwa hiyo kutokana na imani hiyo waamini wengine wanakubali kuwa yawezekana lugha nyingi zinazoonekana leo ni tokeo la mnara wa Babeli.
Kama hivyo haitoshi, Wamisri wanachagiza nadharia hii kwakuwa na Mungu wao aliyeitwa Thoth ambaye ni Mungu wa Lugha. Wahindu walihusisha uwezo wa mwanadamu wa kuzungumza na mungu wao wa kike aliyeitwa Brahma ambaye kwa imani yao Brahma ndiye Mungu muubaji wa ulimwengu lakini lugha alipewa mwanadamu kutoka kwa mke wake aliyeitwa Sarasvati.
Suala la msingi katika nadharia hii ni kwamba lugha za mwanadamu zinakianzo kimoja na ndio maana wanaisimu wa baadaye wamekuwa wakizungumzia suala la sarufi bia. Udhaifu wake nikwamba zinashindwa kujibu maswali kama- kwanini lugha nyingine zinazuka tu sikuhizi bila ya kuwa nazo zimetoka kwa Mungu. Vile vile, mtazamo huu haujajikita katika tafiti za sayansi ya lugha yaani Isimu, pia haujafuata taratibuza kiuchunguzi wa kiisimu ambayo ndio sayansi ya lugha.

4.2.            Nadharia ya Wigo wa Sauti za Asili/ kianzo asilia

Nadharia nyingine inayoeleza juu ya asili ya lugha ni ile ya Wigo. Kwa mujibu wa Yule (2010), nadharia hii inashikilia msimamo kuwa sauti za awali kabisa za lugha ya binadamu ni matokeo binadamu kuiga sauti asilia ambazo wanawake na wanaume walizisikia katika mazingira yao. Nadharia hii inapigiwa upatu na baadhi ya maneno ambayo yanatokana na sauti asilia za milio ya vitu kama vile vitu vinapodondoka, au kugongana ambayo huitwa onomatopoeia.
Pamoja na uthibitisho unaoweza kutolewa kwa maneno hayo machache ambayo huenda kila lugha inayo, bado kuna udhaifu katika nadharia hii. Nadharia hii haijitoshelezi kwakuwa kuna maneno mengi tu mbayo kwa asili yake hayatokani na milio ya vitu, kama majina, na vitenzi ambayo ni matokeo ya njia nyingine za uundaji wa maneno na siyo uigo wa sauti asilia.

4.3.            Nadharia ya mchangamano wa na mahusiano ya kijamii

Nadharia hii inashikilia msimamo kuwa, wakati Fulani katika maisha ya mwanadamu, alihitaji msaada wa mwanadamu mwingine katika kufanya kazi. Katika kazi hizo binadamu hao walitoa milio na sauti mbali mbali za kuhamasishana. Kutokana na sauti hizo yasemekana ndipo lugha ilipoanza. Hatahivyo nadharia hii inatupa wazo moja muhimu kwamba maendeleo ya lugha ya mwanadamu yanatokana na mazingira ya kijamii alimoishi mwanadamu. Kwa hiyo wanadamu lazima waliishi katika makundi ya kijamii, kama hilo linaweza kukubalika, lazima tukubali kuwa yamkini kulikuwa na kanuni maaumu ambazo zilitawala mfumo wao wa mawasiliano katika maisha yao na mahusiano yao ya kijamii.
Pamoja na hayo, nadharia hii bado inatunyima majibu ya swali letu la msingi juu ya asili ya hizo sauti zilizozalishwa. Kama chanzo cha lugha ni mahusiano ya kijamii, kuna wanyama wengine wanaoishi katika makundi makundi kama tumbili na ngedere lakini mawasiliano haya hayaendelei kuwa matamshi ya lugha.

4.4.            Nadharia ya Ki-maumbile ya Mwanadamu

Badala ya kuchunguza asili ya sauti za mwanadamu na kutoa tamko kuwa huenda ndizo chanzo na asili ya lugha ya mwanadamu, nivema tukaangalia sifa za kimaumbile alizonazo mwanadamu. Uchunguzi huu unajikita katika zile sifa ambazo viumbe wengine (wanyama) hawana (Rejea Yule, 2010). Msimamo wa nadharia hii ni kuwa tofauti ya kimaumbile kati ya mwananadamu na wanyama kama Nyani ndiyo uliokuwa chanzo cha lugha y mwanadamu.

5.0.            Utangulizi wa Isimu

5.1.            Isimu ni nini?

Fasili iliyozoeleka na pengine inakubalika na wataalamu wengi wa lugha ni kuwa Isimu ni elimu ya sayansi ya lugha. Ni uchunguzi wa kisayansi na wa kimantiki kuhusu vipengele na sifa mbali mbali za lugha. Swali ambalo tunaweza kujiuliza ni kwamba; “Kwa nini isimu ni sayansi?” Verma et al (1989:29), wanasema kuwa isimu ni sayansi kwakuwa hufuata na kutumia mbinu za kimsingi za utafiti wa kisayansi. Mbinu hizo ni kama zifuatazo:
i.                    Uchunguzi uliodhibitiwa
ii.                  Uundaji wa mabunio
iii.                Uchanganuzi
iv.                Ujumlishi/ujumuishi
v.                  Utabiri
vi.                Majaribio na uthibitishaji
vii.              Urekebishaji au ukataaji wa mabunio

5.2.            Misingi ya kisayansi

Kwa hatua hizi, tunathubutu kusema kuwa isimu haichunguzi lugha kiholela tu bali kwa mwelekeo maalumu. Katika kuchunguza lugha wanaisimu hutumia misingi ya kisayansi kama zifanyavyo sayansi nyingine, misingi hii ni kama vile; uwazi, utaratibu na urazini.

5.2.1        Uwazi

Dhana hii inamaanisha kuwa maswala katika isimu huelezwa kwa udhahiri usio na utata wowote. Hoja huelezwa bila kuleta vugu vugu lolote la kimaana hii ni kinyume na mawasiliano yasiyo kisayansi.

5.2.2.      Utaratibu

Habwe na Karanja, (2003) wanaeleza kuwa utaratibu na uwazi ni dhana zinazokaribiana sana. Bila kuwa na uwazi ni vigumu kuwa na utaratibu na kinyume chake. Utaratibu ni kufanya jambo kwa mpangilio mzuri wenye kubainika. Utaratibu unaweza kuhusisha wakati, idadi, umuhimu na hata ukubwa

5.2.3.      Urazini/Uhoromo

Mtafiti hatakiwi kughosha hisia zake na kuzitumia kueleza jambo fulani. Hii ina maanisha kuwa mtafiti hatakiwi kuruhusu hisia zake kuathiri utafiti wake wa kisayansi hatakama suala la mguso linatafitiwa. Katika utafiti, kitu chamsingi ni data na matokeo ya uchunguzi yanayotokana na data zilizotumika. Utetezi wa matokeo vile vile lazima utokane hatua madhubuti za kisayansi na kiutafiti.

5.3.      Upeo wa Isimu

Habwe na Karanja, (2003) wansema kuwa, katika kushughulikia lugha wanaisimu hujaribu kujibu maswali kama vile:
i.                    Lugha ni nini?
ii.                  Asili ya lugha ni nipi?
iii.                Lugha hufanya kazi namna gani katika mawasiliano?
iv.                Lugha inahusiana namnagani na asasi nyingine maishani?
v.                  Kujua lugha ni nini?
vi.                Namna gani mtoto anajifunza lugha?
vii.              Kwa nini lugha hubadilika?
viii.            Lugha zinatofautiana kwa kiasi gani?
Hivyo katika kujaribu kujibu maswali haya, mwanaisimu hujikuta akiwa na kazi ya kutimiza majukumu yafuatayo:
i.                    Kueleza maana na asili ya lugha
ii.                  Kuchambua muundo wa lugha
iii.                Kueleza uhusiano kati ya lugha na asasi nyingine za mwanadamu
iv.                Kuibua nadharia mbali mbali za lugha

5.4.      Istilahi za msingi katika uchunguzi wa kiisimu

Katika sehemu hii ni muhimu kwa kila msomaji wa lugha au mwanaisimu kuzifahamu na kuweza kuzitofautisha istilahi zifuatazo kama zinavyotumika katika taaluma ya lugha.

5.4.1.      Sikronia na Daikronia

Katika sinkronia, lugha huchunguzwa kwa kuangalia namna ilivyotumika katika kipindi fulani maalumu cha wakati bila kujali mabadiliko yake yanayotokea. Kwa upande mwingine katika daikronia lugha huchunguzwa katika mtazamo wa historia ya mabadiliko yake. Hapa wanaisimu hulinganisha lugha kwa kuangalia tofauti zake zinazotokana na mabadiliko ya kihistoria na kuzielezea tofauti hizo. Kwa mfano mabadiliko yaliyoko kati ya Kiswalihi cha kale (mathalani miaka ya 1900) na Kiswahili cha sasa yanawezwa kuelezewa kifonolojia, kisarufi, na kimaana.

5.4.2.      Umilisi (langue) na utendi (parole)

Umilisi ni ujuzi alio nao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi alio nao mjua lugha ambao upo katika ubongo wake. Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha hiyo husika. Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi, zisizosahihi na kupambanua sententi zenye utata. Ujuzi huo humwezeha kupuuza makosa ya kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, kukatisha sentensi n.k.(Rubanza, 2003).
Utendi (aji) ni kile asemacho mjua lugha katika muktadha wa mawasiliano ikiwa ni pamoja na makosa ya kiutendaji ya bahati mbaya nay ale ya kukusudiwa. Vile vile tunaweza kusema ni udhihirikaji wa ujuzi wa lugha alionao mjua lugha.

5.4.3.      Utumizi (functionalism) na Urasmi (formalism)

Utumizi au isimu tumizi ni elimu inayohusu muundo wa lugha kwa kurejelea kazi zake za kijamii katika mawasiliano. Inamchukulia mtu binafsi kama kiumbe-jamii na kuchunguza namna anavyojifunza lugha na kuitumia katika mawasiliano na wanajamii wenzake. Urasmi au isimu rasmi ni elimu ya maumbo dhahania ya lugha na mahusiano yake ya ndani. Huzingatia maumbo ya lugha kama uthibitisho wa kimalimwengu bila kuzingatia namna jamii inavyowasiliana.

5.4.4.      Uelezi na Uelekezi

Uelezi (isimu elezi) ni mtazamo ambao huelezea ukweli wa lugha jinsi ilivyo na inavyotumika na jamiilugha husika. Na siyo namna inavyotakiwa kutumika. Isimu elezi haiweki kanuni ngumu au sheria ngumu zozote zinazotokana na mawazo ya mtu juu ya lugha fulani bali huelezea lugha kwa kuangalia namna lugha hiyo inavyojidhihirisha yenyewe. Huelezea sheria na kanuni ambazo mzungumzaji mzawa ameziweka kichwani na zinazoakisi uwezo wake wa lugha. Kwa kifupi, haielezi wala kuagiza namna mtu anavyotakiwa kutumia lugha bali namna lugha ilivyo na inavyotumika na wamilisi wa lugha hiyo.
Uelekezi (isimu elekezi) ni mtazamo unaojaribu kuweka kanuni za usahihi wa namna watu wanavyotakiwa kutumia lugha.

5.5.      Matawi ya Isimu

5.5.1.      Isimu ubongo – ni tawi la isimu linalochunguza mahusiano kati ya lugha na michakato ya kiakili (ubongo), uzalishaji wa matamshi katika ujifunzaji wa lugha. Msingi mkubwa katika tawi hili la isimu ni kuwa mchakato wa uzungumzaji huanzia katika akili ya mtu. Hivyo mwanaisimu ubongo hujaribu kutafitina kueleza ni nini hasa kinatokea katika ubongo ambacho kinamwezesha mwanadamu kuzungumza. Pia hutafiti na kueleza matatizo katika lugha yanayotokana na matatizo katika ubongo wa mwanadamu.

5.5.2.      Isimu jamii - Isimu Jamii (social linguistcs) - ni tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia. King’ei (2010), anaeleza kuwa, kwanza lugha ni zao la jamii, na ni kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika. Pili, lugha hutumiwa na jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo isimu jamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha.

5.5.3.      Isimu anthropolojia – tawi hili la isimu hukijita katika kutafiti na kueleza historia ya na miundo ya lugha ambazo bado hazijaandikwa.

5.5.4.      Isimu kompyuta – huchunguza matumizi ya kompyuta katika kuchakata na kuzalisha lugha ya mwanadamu. Ni tawi ambalo kwa hakika si la muda mrefu na linatokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia hasa baada ya uvumbuzi wa kifaa kama kompyuta.

5.5.5.      Isimu tumizi – huchambua na kueleza matumizi ya nadharia mbali mbali za lugha na maelezo ya kufundishia lugha.

5.6.      Ujuzi wa Lugha na Mjua Lugha

Swali la msingi tunaloweza kujiuliza ni kuwa, “mjua lugha ni nani?” na “kujua lugha ni nini?” Katika hali ya kawaida imekuwa ni mazoea mtu kusema “mimi ninajua lugha” au “hawa hawajui lugha”. Lakini je ni nini hasa kujua lugha? Majibu yake ni kama yafuatayo:
i.                    Kujua lugha ni uleuwezo wa kutabua na kubainisha sauti pekee za lugha
ii.                  Kujua lugha ni kujua namna sauti hizo zinavyoungana
iii.                Kujua lugha ni kujua namna maneno yanavyowezwa kuundwa na kugawanywa
iv.                Kujua lugha ni kujua namna maneno yananyoungana kutengeneza tungo
v.                  Kujua lugha ni kujua naana ya maneno na visemo mbali mbali vya kugha husika
vi.                Kujua lugha ni kuweza kutumia lugha hiyo katika muktadha wa mawasiliano
Kwa maelezo hayo tunakuwa tumejibu swali la kuwa kujua lugha ni nini. Swali la mjua lugha ni nani hapa linakua sitata tena kwani mtu anaye kuwa anasifa zote hizo hapo juu tunasema huyu ni mjua lugha.

6.0.            Muundo wa Lugha

Hoja kuwa lugha ni mfumo inamaanisha kuwa lugha inamuundo unaohusisha viambajengo mbali mbali. Viaambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha. Viambajengo hivi, hushughulikiwa na tanzu tofauti tofauti za isimu muundo. Tanzu hizi ni Fonetiki na fonolojia – ambazo hushughulikia sauti za lugha, mofolojia – ambayo hushughulikia maumbo ya maneno na jinsi lugha inavyounda maneno yake, sintaksia – ambayo hushughulikia namna senteni zinavyoundwa na kanuni zinazotawala uundwaji wake na mwisho ni semantiki – ambayo hushughulikia maana katika viwango vyote vya vya lugha tulivyo vitaja. Kwa ujumla tanzu hizi zote zinahusiana kwa ukaribu, zina shirikiana, na kukamilishana. Tazama mchoro ufuatao:


 
MAREJEO

Bloch, B. na Trager, G. (1942). Outline of Linguistic Analysis. Waverly Press.
Chomsky, Noam (1957), Syntactic Structures, The Hague: Mouton.
Cook, V.J. (1969), 'The analogy between first and second language learning', International Review of Applied Linguistics, VII/3, 207-216
Habwe, J na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Phoenix Publishers
King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimu Jamii. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tanzania.
Mario A. P. and Gaynor, F. (1954). A Dictionary of Linguistics. Philosophical Library. New York.
OUT na Rubanza, Y.I. (2003). Sarufi Mtazamo wa Kimuundo. The Open University of Tanzania.
Sapir, E. (1921). An introduction to the Study of Speech. New York: Harcourt, Brace, 1921; Bartleby.com, 2000. www.bartleby.com/186/.
Todd, L., (1987). An Introduction to Linguistics. Essex: Longman Group Limited.
TUKI. (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Yule, g. (2010). The Study of Language (4th edition). Cambridge University Press.