KSW 101: UTANGULIZI WA
LUGHA NA ISIMU
Muhadhara wa kwanza
MAANA YA LUGHA
1.0.
Lugha ni nini?
Mtu anapouliza swali
hili (Lugha ni nini?) inaweza kuonekana kana kwamba ni swali la kijinga. Labda
kwa sababu huwa hatupendi kutilia maanani katika vitu ambavyo tunadhani ni vya
kawaida. Kwa bahati mambo hayapo kama tunavyoweza kuyaona au kuyatafakari. Kwa
maana hiyo basi, hata swali la kwamba “lugha ni nini?” siyo rahisi na wala siyo
la kawaida kama ambavyo tunaweza kulichukulia. Kwa maelezo hayo tunaweza
kufasili dhana ya lugha kwa mitazamo miwili: Mtazamo finyu (narrow conception) na Mtazamo mpana (Broad conception).
1.1.
Mtazamo Finyu:
i.
Lugha ni chombo cha mawasiliano
Kuitazama lugha kama tu
chombo cha mawasiliano kunawezesha ufahamu wa kawaida. Kwa maana hiyo, bado
kuna taarifa muhimu zinakosekana katika fasili na hii inatupatia mapungufu ya
fuatayo: kwanza, kueleza lugha kama chombo cha mawasiliano ni kueleza kazi ya
lugha na sio lugha yenyewe. Pili, kama mtu atapiga ngoma ili kuwaita watu na
watu wakaja basi milio ya ngoma itakuwa ni lugha. Na kwamaana hiyo kila
kitakacho wawezesha watu kuwasiliana kitakuwa ni lugha. Kama lugha ni chombo tu
cha mawasiliano, maana yake hakuna tofauti yoyote kati ya kuzungumza na milio
mbali mbali kama honi ya gari, filimbi ya refa uwanjani, au kengere ya kanisani
au hata sauti inayotokana na kugonga mlango wakati mtu anabisha hodi. Hivyo
jambo hili sio la kweli na linatupeleka mbali zaidi na kutufanya tuanze
kuitazama fasili ya lugha kwa mtazamo mwingine zaidi – mtazamo mpana.
1.2.
Mtazamo Mpana.
Katika mtazamo huu
kunawanaisimu wengi ambao wamejaribu kutoa fasili zao mbali mbali. Baadhi ya
fasili hizo ni kama zifuatazo:
i.
Todd
(1987) anasema lugha ni mfumo wa ishara ambazo kwazo watu
huwasiliana.
ii.
Kamusi
ya Isimu na lugha (1990) inaeleza kuwa lugha ni mfumo wa
sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii wenye utamaduni unaofanana ili
kuwasiliana.”
iii.
Cook,1969:12
anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa sauti
nasibu na ishara za kisarufi ambazo kwazo watu wa jamii Fulani ya lugha
huwasiliana na kupokezana utamafuni wao.
iv.
Bloch
and Trager (1942): “A language is a system of arbitrary vocal symbols by
means of which a social gorup co-operates”.
[“Lugha ni mfumo wa sauti za
nasibu ambazo kwazo makundi ya kijamii hushirikiana”]
v.
Noam
Chomsky(1957): “Language is a set of finite number sentences, each finite in
lingth and constructed out of a finite set of elements”
[“Lugha ni seti ya
idadi ya sentensi zinazojitosheleza, kila idadi inajitosheleza kwa urefu na
hujengwa kutokana na seti za elementi zinazo jitosheleza”.]
vi.
Michael
Halliday (2003): “A language
is a system of meaning- a semiotic system”
[“Lugha ni mfumo wa maana –
yaani mfumo wa ishara (semiotic system)”]
vii.
Muharrem
Ergin(1990): “Language is a
natural means to enable communication among people, a living entity that it has
its own peculiar laws, by means of which alone can it develop, a system of
contracts whose foundation was laid in times unknown, and a social institution
interwoven with sounds”.
[“Lugha ni njia ya asili ya
kuwezesha mawasiliano miongoni mwa watu, ni chombo hai yaani chenye sheria zake
za pekee ambazo kwazo peke yake hujijenga, ni mfumo wa makubaliano ambao
misingi yake iliwekwa katika wakati usiojulikana, na ni taasisi ya kijamii
ambayo imechangamana na sauti.]
viii.
Language: “The
system of arbitrary vocal symbols we use to encode our experience of the world”
[Lugha ni
mfumo wa sauti za nasibu ambazo tunazitumia kusimba uelewa na uzoefu wetu wa
ulimwengu.]
ix.
Nae Sapir
(1921:7) anasema: “Language is
a purely human and non-instinctive method of communicating ideas, emotions and
desires by means of voluntarily produced symbols.”
[Lugha ni njia
ya mawasiliano ambayo ni maalumu kwa mwanadamu na isiyo silika ambayo hutumiwa
kuwasilisha mawazo, hisia na matakwa kwa kutumia ishara ambazo hutolewa kwa
hiyali].
x.
Mario Pei & Frank Gaynor (1954) Kamusi ya Isimu (A Dictionary of Linguistics)
anasema: Language is a system of
communication by sound, i.e., through the organs of speech and hearing, among
human beings of a certain group or community, using vocal symbols possessing
arbitrary conventional meanings.
[Lugha ni mfumo wa
mawasiliano kwa njia ya sauti, yaani, kwakutumia alasauti na kusikia, miongoni
mwa binadamu wa kundi fulani au jumuiya kwa kutumia ishara-sauti ambazo maana
zake hueleweka kwa unasibu tu.
2.0.
Tathmini ya Fasili za Lugha
Ukichunguza fasili hizi na nyingine nyingi ambazo hazijatolewa hapa
utagundua kuwa swali letu tuliloliuliza hapo mwanzo yaai “Lugha ni nini?” sio
swali la kijinga wala sio swali rahisi kulijibu. Hivyo basi, kutokana na fasili
hizo tunaweza kusema kuna maana mbali mbali za lugha kulingana na mzingira,
mazoea, taaluma na hata mahala mtu alipobobea kitaaluma. Lakini, pamoja na
tofauti hizi mbali mbali zinazojitokeza, tunaona kuna mambo kadhaa ya msingi
ambayo takribani wataalamu wote wanayagusia wanapofasili dhana ya ‘lugha’.
Mambo hayo ni kama yafuatayo: Lugha ni
mfumo, Lugha ni mfumo wa sauti nasibu, Lugha ni maalumu kwa binadamu, Lugha ni
mfumo wa ishara, Lugha hutumia sauti, Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano.
Kimsingi mambo haya ndiyo yanayogusiwa katika fasili hizi. Lakini ikumbukwe
kuwa, sio kila fasili zilizotajwa hapo juu zinajumuisha vipengele vyote hivi.
La hasha! Fasili moja inaweza ikawa inakipengele kimoja wapo au viwili kati ya
hivi. Kila kimoja kinaelezewa hapa chini kama ifuatavyo.
2.1.
Lugha ni mfumo
Ishara zinazotumiwa katika lugha zinampangilio wenye kutawaliwa na sheria
na unaruwaza zinazotambulika na watumiaji wa lugha hiyo. Kila lugha ya
mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa
maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya
neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai,
vishazi, sentensi na aya.
Katika muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni
na sheria zinazidhibiti mfuatano wa kila kipashio. Kuna kanuni zinazo dhibiti
mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa
sentensi. Hivyo basi, mtu hawezi kuunganisha tu sentensi kwa matakwa yake bila
kujali kanuni hizi, akifanya hivyo atasababisha kutokea kwa kitu ambacho siyo
lugha na wala hakikubaliki katika lugha. Kwa maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni
mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa basi kuna kuwa
hakuna utimilifu wa lugha husika. Lugha inaonesha utaratibu katika mahusiano ya
viunzi vya lugha. Sheria hizi zinazotawala mpangilio wa viunzi vya lugha hiyo
ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana.
2.2.
Lugha ni mfumo wa sauti nasibu (Unasibu katika lugha ya
mwanadamu)
Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja
kati ya neno (mathalani kiti) na kitu chenyewe tunachotumia kukalia (maana na
kilejelewa). Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano
wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa.
Tazama mchoro ufuatao:

Katika picha inayoonekana hapo juu kuna neno ‘mti’ na mmea wenyewe ambao
umebatizwa jina hilo. Katika hali halisi hakuna watu waliokaa nakusema kuanzia
leo huu utaitwa mti. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya neno “MTI” an
umbo linalomaanishwa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutokana na
lugha na lugha. Hii ndiyo maana Waingereza wataita tree, Wahehe wataita mubiki, Wasukuma
wataita mpiki n.k. Ukweli kwamba
hakuna uhusiano wa asili kati ya umbo la neno na maana ambazo umbo hilo
linapewa ndiyo sababu inayofanya kuwe na namnatofauti ya kuuelezea ulimwengu.
Ferdinand de Saussure katika kile alichokiita ishara za kiisimu anabainisha sawia
mbili za mahusiano haya; kwanza ni “signifie”
ambacho ni kiashiria yaani umbo la kifonolojia (kutamkwa) au kiothografia
(kuandikwa) na ambalo huwakilisha dhana Fulani. Kitu cha pili ni “significant” ambacho ni kiashiriwa
ambacho ni kitu chenyewe kilicho katika ulimwengu halisi wa vitu na dhana.
Hivyo basi, uhusiano kati ya kiashiria na kiashiriwa ndio unlio wa unasibu.
2.3.
Lugha ni maalumu kwa mwanadamu.
Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba
hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu anauwezo wa kuzungumza na kutumia
lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa Fulani za lugha za binadamu ambazo
hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege,
mbwa, nyuki, tumbili wanawea kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au
ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama
hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu anauwezo wa kujifunza lugha
mbali mbali na kutumia katika mazingira yake na sio wanyama. Kwa mfano, ukimtoa
mbwa Tanzania na kumpeleka Japani, atatoa sauti ile ile sawa na mbwa wa Japani
kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.
2.4.
Lugha ni mfumo wa ishara
Uishara wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa / huhusishwa na
vitu, matendo, mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale
tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika
muktadha wa mawasiliano. Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo
wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu
vinavyowakilisha.
2.5.
Lugha hutumia sauti
Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti.
Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na
uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu.
Tafiti zinathibitisha kuwa mfumo wa maandishi umekuja baadaye sana katika
maendeleo ya binadamu na kwamba hutumika tu kuwasilisha yale yanayosemwa kwa
kutumia kinywa cha mzungumzaji. Vile vile, ukweli kwamba binadamu anapozaliwa
huanza kujua lugha ya mahala anapokua na kuishi kabla ya kufahamu kuandika,
unatuthibitishia kuwa kiunzi (msingi) cha lugha ni sauti.
Kwa ujumla, kuna sababu kuu tano zinazotuwezesha kukubaliana kuwa msingi
wa lugha ni sauti za kutamkwa.
i.
Mtoto
hujifunza kuzungumza kablra hajajifunza kusoma na kuandika
ii. Mtoto hujifunza lugha moja kwamoja bila kufikiri
kadiri anavyokuwa.
iii. Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
iv. Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
v. Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza
kuliko kuandika
vi.
Kuna mambo
mengi ya muhimu katika sauti z lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa
kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo,
toni, mkazo, kidatu, haya ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi
kuwasilishwa kisawa sawa kwakutumia maandishi (Habwe na Karanja, 2003).
2.6.
Lugha ni kwaajili ya mawasiliano
Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi
kuvifanya. Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio
yetu, kucheza, kufanya kazi n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha
ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.
2.7.
Fasili ya jumla
Hivyo basi, baada ya kuchunguza fasili hizo za lugha na vipengele
vinavyojibainisha kwenye kila fasili mojawapo, tunaweza kusema kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu
zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kilasiku
kueleza hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.
3.0.
Tabia za lugha ya binadamu ainazoitofautisha na aina nyingine
za mawasiliano
Tumekwisha elezwa hapo awali kuwa lugha ni maalumu kwa binadamu tu na
kwamba hakuna kiumbe yeyote ambaye si mwanadamu mwenye uwezo wa kujua,
kujifunza na kutumia lugha zaidi ya binadamu. Jambo hili linatupelekea
kuzitathmini sifa au tabia za lugha ya mwanadamu. Kimsingi sifa/tabia hizi
ndizo zinazoitofautisha lugha ya mwanadamu na aina nyingine za mawasiliano
zitumiwazo na wanyama.
3.1.
Unasibu
Kama tulivyokwisha eleza mwanzo, unasibu wa lugha ya ninadamu unaangaliwa
katika mambo yafuatayo:
i.
Binadamu
hazaliwi na lugha, anakutananayo kwa unasibu tu
ii.
Hakuna
uhusiano wa moja kwa moja au wa asili kati ya kitaja (neno kama umbo la kiisimu)
na kitajwa (kitu au umbo linalomaanishwa au maana). Uhusiano wake niwa unasibu
na unatokana na makubaliano ya watumia lugha.
iii.
Hata
makubaliano haya ya kwamba kitu kiitwe au dhana fulani iitwe na kuelezwa kwa
namna fulani ni ya nasibu tu. Hapa tunamaanisha kwamba hakuna mkutano au kikao
ambacho binadamu amewahi kukaa akasema mathalani neno “chuki” limaanishe hali ya kuto kumpenda mtu au neno “upendo” limaanishe hali ya kuonesha
huba kwa mtu.
iv.
Kila
jamiilugha ina namna yake ya kuufasili na kuuelezea ulimwengu kwa lugha yake
ambayo inatofautiana na jamiilugha nyingine.
3.2.
Uzalikaji au Ubunifu
Uzalikaji katika lugha ya binadamu unajidhihirisha katika mambo
yafuatayo:
i.
Uwezo wa
mwanadamu kubuni na kuunganisha maneno na miundo mbali mbali ya tungo bila
kikomo.
ii.
Uwezo wa
mwanadamu kutunga na kuzielewa tungo mbali mbali ikiwa ni pamoja na zile ambazo
hajawahi kuzisikia wala kuzitunga.
iii.
Uwezo wa
mwanadamu kuelewa tungo zilizotungwa na watu wengine na kufahamu maana ya
kisemantiki na ile ya kipragmatiki.
iv.
Uwezo wa
mwanadamu kuzielewa tungo sahihi na zile zisizo sahihi
Hivyo uwezo huu unatofautiana na aina nyingine ya mawasiliano inayotumiwa
na wanyama wengine, kwamfano, “nyenje ni myama mwenye milio au ishara nne za
kuchagua ili awasiliane, tumbili ana miito sita tu. Hivyo wanyama wote hawa
wanaidadi isiyobadilika ya milio na sauti au ishara na hawana uwezo wa kubuni
namna nyingine ya kuwasiliana au kubuni milio mingine ya kuwasiliana.
3.3.
Uambukizaji
wa utamaduni
Lugha ya mwanadamu inauwezo wa kuambukiza utamaduni kutoka katika kizazi
kimoja kwenda kizazi kingine au kutoka katika jamiilugha moja kwenda katika
jamiilugha nyingine. Ieleweke kuwa, uwezo huu wa kuambukiza maarifa ya lugha
hufanyika kwa njia ya kusoma au kujifunza na sio kurithi. Kwa mfano, mtu
anaweza kurithi maumbile kutoka kwa wazazi wake, mathalani aina ya nywele, aina
ya macho, lakini mtu hawezi kurithi lugha. Lugha inamfikia kwa kuambukizwa
katika jamiilugha anayokulia. Yatupasa tukumbuke kuwa, ingawa mwanadamu
anazaliwa na uleuwezo (kitengo cha lugha) wa kujifunza lugha “Language Acquisition Device” kama
anavyoeleza mwanaisimu Noam Chomsky, lakini hazaliwi na lugha. Hii ndiyo sababu
mwanadamu anaweza kujifunza lugha yoyote ile na kwa wakati wowote maadamu yupo
katika mazingira na hali ya kawaida na saidizi.
3.4.
Uwili (utamkaji pamwe)
Lugha ya mwanadamu imepangwa katika viwango viwili ambavyo vinashirikiana
na kukamilishana. Kiwango cha kwanza ni kile kiwango cha utamkaji wa sauti au
utoaji wa sauti kama; /n/, /m/, /g/, /t/, /k/, /a/, /e/, /o/ kwa kutumia
alasauti mbali mbali. Sauti hizi zikisimama peke yake hazina maana yoyote, ni
kama milio tu kama kupiga chafya, au kekele zinazotokana na kuburuza meza
kwenye sakafu au kelele za injini ya piki piki. Sauti hizi zinapounganishwa
(kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za lugha husika) tunapata maneno yenye
maana ambapo tunapata kiwango kingine cha pili cha maana. Sifa ya uwili
inadhiririsha sifa ya uwekevu katika lugha ya mwanadamu kwani kwa kutumia sauti
hizi chache mzungumza lugha anaweza kutoa au kuzungumza sentensi nyingi au
tungo nyingi na zenye maana tofauti tofauti bila kikomo.
Suala jingine la msingi ni kwamba, tunaposema kuwa lugha imegawanyika
katika viwango viwili, kiwango cha sauti na kiwango cha maana haimaanishi kwamba
binadamu anatumia viwango hivi kiupeke peke. Hata sikumoja mwanadamu hasemi
kwamba sasa naanza kutamka sauti, mathalani, baba halafu ndiyo niweke maana yake. La hasha! Binadamu hutamka kwa
maramoja sauti pamoja na maana vikiwa vimebebana ndani kwa ndani (hutamka sauti
pamwe na maana). Yaani, wakati anatamka sauti na kuziunganisha ndiyo wakati
anaambatanisha na maana ndani yake. Hii ndiyo sifa ua uwili katika lugha ya
mwanadamu.
3.5.
Uhamisho au Urejelezi
Uhamisho ni sifa ya lugha ya mwanadamu inayomaanisha
kwamba lugha ya mwanadamu inaweza kutumika katika kuzungumzia au kurejelea kitu
ambacho hakipo katika upeo wa macho ya mzungumzaji kiwakati na kimazingira.
Tofauti na mawasiliano ya wanyama, binadamu anaweza kuzungumza juu ya matukio
yaliyopita, matukio yajayo, na hata yale anayoyatarajia kufanya kwa kutumia
lugha. Kwa mfano, myana kama ng’ombe hawezi kuelezea kwa njia yake ya
mawasiliano, aina ya chakula alichokula jana, au anachotamani kula, au
anachotarajia kula, au kwa nini jana alikwenda kunywa maji, au hata kujua
sababu ya kuumia. Lakini mambo haya binadamu anayaweza kwa kutumia lugha yale
ya asili. Hii ndiyo sifa inayoitwa uhamisho au urejelezi (displacement).
3.6.
Uwezo wa kubadilishana taarifa/Ubadilishanaji taarifa
Sifa hii inamaanisha kuwa binadamu wenyewe kama
watumia lugha wanauwezo wa kubadilishana taarifa. Kila mmoja wao anaweza kuwa
mtumaji au mpokeaji wa taarifa kwa kutumia lugha.
3.7.
Upeke
Lugha hundwa na viunzi vidogo vidogo ambavyo ni peke
peke na haipo katika mfululizo. Kila kipashio kinachotumika kuunda tungo za
lugha kipo peke peke na kinaweza kuunganishwa na vingine kupata muundo wa juu
mkubwa zaidi. Hivyo, lugha inawezwa kugawanywa tena kwa kukusayna vipashio
hivyo kuunda tungo kubwa zaidi.
4.0.
Asili ya Lugha
Hakuna maafikiano kati
ya wanaisimu juu ya wapi, lini, namna gani na nani hasa alianzisha lugha. Hii inatokana
na ukweli kwamba binadamu alianza kuishi tangu kale wakati ambapo hata hivyo
bado hauja julikana. Suala ambalo lina uhakika ni kuwa lugha inatumiwa na
mwanadamu na kila jamii ina lugha yake. Hata hivyo kuna nadharia mbali mbali
zinazoeleza chanzo na asili ya lugha. Baadhi ya nadharia hizo ni kama
zifuatazo:
4.1.
Nadharia ya UUngu/mtazamo wa kidini
Msingi wa nadharia hii
ni kwamba lugha iliumbwa na Mungu na akapewa mwanadamu kwa nguvu za Mwenyezi
Mungu. Nadharia hii inaeleza kuwa, haja ya Mungu kuwasiliana na kiumbe wake
Binadamu ndiyo iliyomfanya aumbe lugha. Inaaminika kuwa Mungu ndiye alikuwa wakwanza
kutumia lugha, aliumba ulimwengu kwa kutumia neno, na kwa neno kila kitu
akiwemo mwanadamu likifanyika. Inaaminika kuwa lugha zote zilitokana na lugha
moja iliyoumbwa na Mungu. Hata hivyo kuna visasili mbali mbali vinavyoeleza
asili ya lugha katika nadharia ya Uungu. Kwanza ni, pale Mungu alipompa Adamu
uwezo wa kuzungumza kwa kuwatajia majina wanyama wote na pale ndipo lugha
ilipoanza (Mwanzo 2:19).
Nadhari hii ya uungu
pia huchagizwa na kisasili kingine cha Wamisri, Wababiloni, na Wahindi. Kwa
mujibu wa kisasili cha Wababiloni, inasemekana hapo kale Mfalme wa Babeli
aliamuru kujenga mnara mrefu ulioitwa Mnara
wa Babeli ili kumfikia Mungu. Kwa lengo hilo Mungu alikasirishwa sana
akaamua kuwachanganya lugha wajenzi wa mnara huo hivyo wakashindwa kuelewana na
hatimaye azma yao ikasitishwa. Kwa hiyo kutokana na imani hiyo waamini wengine
wanakubali kuwa yawezekana lugha nyingi zinazoonekana leo ni tokeo la mnara wa
Babeli.
Kama hivyo haitoshi,
Wamisri wanachagiza nadharia hii kwakuwa na Mungu wao aliyeitwa Thoth ambaye ni Mungu wa Lugha. Wahindu
walihusisha uwezo wa mwanadamu wa kuzungumza na mungu wao wa kike aliyeitwa
Brahma ambaye kwa imani yao Brahma ndiye Mungu muubaji wa ulimwengu lakini
lugha alipewa mwanadamu kutoka kwa mke wake aliyeitwa Sarasvati.
Suala la msingi katika
nadharia hii ni kwamba lugha za mwanadamu zinakianzo kimoja na ndio maana
wanaisimu wa baadaye wamekuwa wakizungumzia suala la sarufi bia. Udhaifu wake nikwamba zinashindwa kujibu maswali kama-
kwanini lugha nyingine zinazuka tu sikuhizi bila ya kuwa nazo zimetoka kwa
Mungu. Vile vile, mtazamo huu haujajikita katika tafiti za sayansi ya lugha
yaani Isimu, pia haujafuata taratibuza kiuchunguzi wa kiisimu ambayo ndio
sayansi ya lugha.
4.2.
Nadharia ya Wigo wa Sauti za Asili/ kianzo asilia
Nadharia nyingine
inayoeleza juu ya asili ya lugha ni ile ya Wigo.
Kwa mujibu wa Yule (2010), nadharia hii inashikilia msimamo kuwa sauti za awali
kabisa za lugha ya binadamu ni matokeo binadamu kuiga sauti asilia ambazo wanawake
na wanaume walizisikia katika mazingira yao. Nadharia hii inapigiwa upatu na
baadhi ya maneno ambayo yanatokana na sauti asilia za milio ya vitu kama vile
vitu vinapodondoka, au kugongana ambayo huitwa onomatopoeia.
Pamoja na uthibitisho
unaoweza kutolewa kwa maneno hayo machache ambayo huenda kila lugha inayo, bado
kuna udhaifu katika nadharia hii. Nadharia hii haijitoshelezi kwakuwa kuna
maneno mengi tu mbayo kwa asili yake hayatokani na milio ya vitu, kama majina,
na vitenzi ambayo ni matokeo ya njia nyingine za uundaji wa maneno na siyo uigo
wa sauti asilia.
4.3.
Nadharia ya mchangamano wa na mahusiano ya kijamii
Nadharia hii inashikilia
msimamo kuwa, wakati Fulani katika maisha ya mwanadamu, alihitaji msaada wa
mwanadamu mwingine katika kufanya kazi. Katika kazi hizo binadamu hao walitoa
milio na sauti mbali mbali za kuhamasishana. Kutokana na sauti hizo yasemekana
ndipo lugha ilipoanza. Hatahivyo nadharia hii inatupa wazo moja muhimu kwamba
maendeleo ya lugha ya mwanadamu yanatokana na mazingira ya kijamii alimoishi
mwanadamu. Kwa hiyo wanadamu lazima waliishi katika makundi ya kijamii, kama
hilo linaweza kukubalika, lazima tukubali kuwa yamkini kulikuwa na kanuni maaumu
ambazo zilitawala mfumo wao wa mawasiliano katika maisha yao na mahusiano yao
ya kijamii.
Pamoja na hayo,
nadharia hii bado inatunyima majibu ya swali letu la msingi juu ya asili ya hizo
sauti zilizozalishwa. Kama chanzo cha lugha ni mahusiano ya kijamii, kuna
wanyama wengine wanaoishi katika makundi makundi kama tumbili na ngedere lakini
mawasiliano haya hayaendelei kuwa matamshi ya lugha.
4.4.
Nadharia ya Ki-maumbile ya Mwanadamu
Badala ya kuchunguza
asili ya sauti za mwanadamu na kutoa tamko kuwa huenda ndizo chanzo na asili ya
lugha ya mwanadamu, nivema tukaangalia sifa za kimaumbile alizonazo mwanadamu.
Uchunguzi huu unajikita katika zile sifa ambazo viumbe wengine (wanyama) hawana
(Rejea Yule, 2010). Msimamo wa nadharia hii ni kuwa tofauti ya kimaumbile kati
ya mwananadamu na wanyama kama Nyani ndiyo uliokuwa chanzo cha lugha y
mwanadamu.
5.0.
Utangulizi wa Isimu
5.1.
Isimu ni nini?
Fasili iliyozoeleka na
pengine inakubalika na wataalamu wengi wa lugha ni kuwa Isimu ni elimu ya sayansi ya lugha. Ni uchunguzi wa kisayansi na wa
kimantiki kuhusu vipengele na sifa mbali mbali za lugha. Swali ambalo tunaweza
kujiuliza ni kwamba; “Kwa nini isimu ni
sayansi?” Verma et al (1989:29), wanasema kuwa isimu ni sayansi kwakuwa
hufuata na kutumia mbinu za kimsingi za utafiti wa kisayansi. Mbinu hizo ni
kama zifuatazo:
i.
Uchunguzi uliodhibitiwa
ii.
Uundaji wa mabunio
iii.
Uchanganuzi
iv.
Ujumlishi/ujumuishi
v.
Utabiri
vi.
Majaribio na uthibitishaji
vii.
Urekebishaji au ukataaji wa mabunio
5.2.
Misingi ya kisayansi
Kwa hatua hizi,
tunathubutu kusema kuwa isimu haichunguzi lugha kiholela tu bali kwa mwelekeo
maalumu. Katika kuchunguza lugha wanaisimu hutumia misingi ya kisayansi kama
zifanyavyo sayansi nyingine, misingi hii ni kama vile; uwazi, utaratibu na urazini.
5.2.1
Uwazi
Dhana hii inamaanisha
kuwa maswala katika isimu huelezwa kwa udhahiri usio na utata wowote. Hoja
huelezwa bila kuleta vugu vugu lolote la kimaana hii ni kinyume na mawasiliano
yasiyo kisayansi.
5.2.2.
Utaratibu
Habwe na Karanja,
(2003) wanaeleza kuwa utaratibu na uwazi ni dhana zinazokaribiana sana. Bila
kuwa na uwazi ni vigumu kuwa na utaratibu na kinyume chake. Utaratibu ni
kufanya jambo kwa mpangilio mzuri wenye kubainika. Utaratibu unaweza kuhusisha
wakati, idadi, umuhimu na hata ukubwa
5.2.3.
Urazini/Uhoromo
Mtafiti hatakiwi
kughosha hisia zake na kuzitumia kueleza jambo fulani. Hii ina maanisha kuwa
mtafiti hatakiwi kuruhusu hisia zake kuathiri utafiti wake wa kisayansi
hatakama suala la mguso linatafitiwa. Katika utafiti, kitu chamsingi ni data na
matokeo ya uchunguzi yanayotokana na data zilizotumika. Utetezi wa matokeo vile
vile lazima utokane hatua madhubuti za kisayansi na kiutafiti.
5.3.
Upeo wa Isimu
Habwe na Karanja,
(2003) wansema kuwa, katika kushughulikia lugha wanaisimu hujaribu kujibu
maswali kama vile:
i.
Lugha ni nini?
ii.
Asili ya lugha ni nipi?
iii.
Lugha hufanya kazi namna gani katika
mawasiliano?
iv.
Lugha inahusiana namnagani na asasi
nyingine maishani?
v.
Kujua lugha ni nini?
vi.
Namna gani mtoto anajifunza lugha?
vii.
Kwa nini lugha hubadilika?
viii.
Lugha zinatofautiana kwa kiasi gani?
Hivyo katika kujaribu
kujibu maswali haya, mwanaisimu hujikuta akiwa na kazi ya kutimiza majukumu
yafuatayo:
i.
Kueleza maana na asili ya lugha
ii.
Kuchambua muundo wa lugha
iii.
Kueleza uhusiano kati ya lugha na asasi
nyingine za mwanadamu
iv.
Kuibua nadharia mbali mbali za lugha
5.4.
Istilahi za msingi katika uchunguzi wa kiisimu
Katika sehemu hii ni
muhimu kwa kila msomaji wa lugha au mwanaisimu kuzifahamu na kuweza
kuzitofautisha istilahi zifuatazo kama zinavyotumika katika taaluma ya lugha.
5.4.1.
Sikronia na Daikronia
Katika sinkronia, lugha huchunguzwa kwa
kuangalia namna ilivyotumika katika kipindi fulani maalumu cha wakati bila
kujali mabadiliko yake yanayotokea. Kwa upande mwingine katika daikronia lugha huchunguzwa katika
mtazamo wa historia ya mabadiliko yake. Hapa wanaisimu hulinganisha lugha kwa
kuangalia tofauti zake zinazotokana na mabadiliko ya kihistoria na kuzielezea
tofauti hizo. Kwa mfano mabadiliko yaliyoko kati ya Kiswalihi cha kale
(mathalani miaka ya 1900) na Kiswahili cha sasa yanawezwa kuelezewa
kifonolojia, kisarufi, na kimaana.
5.4.2.
Umilisi (langue) na utendi (parole)
Umilisi
ni ujuzi alio nao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi alio nao mjua lugha
ambao upo katika ubongo wake. Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha hiyo
husika. Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi, zisizosahihi na
kupambanua sententi zenye utata. Ujuzi huo humwezeha kupuuza makosa ya
kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, kukatisha sentensi
n.k.(Rubanza, 2003).
Utendi
(aji) ni kile asemacho mjua lugha katika muktadha wa
mawasiliano ikiwa ni pamoja na makosa ya kiutendaji ya bahati mbaya nay ale ya
kukusudiwa. Vile vile tunaweza kusema ni udhihirikaji wa ujuzi wa lugha alionao
mjua lugha.
5.4.3.
Utumizi (functionalism) na Urasmi (formalism)
Utumizi
au isimu tumizi ni elimu inayohusu muundo wa lugha kwa
kurejelea kazi zake za kijamii katika mawasiliano. Inamchukulia mtu
binafsi kama kiumbe-jamii na kuchunguza namna anavyojifunza lugha na kuitumia
katika mawasiliano na wanajamii wenzake. Urasmi au isimu rasmi ni elimu ya maumbo dhahania ya lugha na
mahusiano yake ya ndani. Huzingatia maumbo ya lugha kama uthibitisho wa
kimalimwengu bila kuzingatia namna jamii inavyowasiliana.
5.4.4.
Uelezi na Uelekezi
Uelezi
(isimu elezi) ni mtazamo ambao huelezea ukweli wa
lugha jinsi ilivyo na inavyotumika na jamiilugha husika. Na siyo namna
inavyotakiwa kutumika. Isimu elezi haiweki kanuni ngumu au sheria ngumu zozote
zinazotokana na mawazo ya mtu juu ya lugha fulani bali huelezea lugha kwa
kuangalia namna lugha hiyo inavyojidhihirisha yenyewe. Huelezea sheria na
kanuni ambazo mzungumzaji mzawa ameziweka kichwani na zinazoakisi uwezo wake wa
lugha. Kwa kifupi, haielezi wala kuagiza namna mtu anavyotakiwa kutumia lugha
bali namna lugha ilivyo na inavyotumika na wamilisi wa lugha hiyo.
Uelekezi
(isimu elekezi) ni mtazamo unaojaribu kuweka kanuni za
usahihi wa namna watu wanavyotakiwa kutumia lugha.
5.5.
Matawi ya Isimu
5.5.1. Isimu ubongo
– ni tawi la isimu linalochunguza mahusiano kati ya lugha na michakato ya
kiakili (ubongo), uzalishaji wa matamshi katika ujifunzaji wa lugha. Msingi
mkubwa katika tawi hili la isimu ni kuwa mchakato wa uzungumzaji huanzia katika
akili ya mtu. Hivyo mwanaisimu ubongo hujaribu kutafitina kueleza ni nini hasa
kinatokea katika ubongo ambacho kinamwezesha mwanadamu kuzungumza. Pia hutafiti
na kueleza matatizo katika lugha yanayotokana na matatizo katika ubongo wa
mwanadamu.
5.5.2. Isimu jamii -
Isimu Jamii (social linguistcs) - ni
tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika
jamii na uhusiano baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika
mazingira tofauti; aina mbali mbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati
ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia. King’ei (2010), anaeleza kuwa,
kwanza lugha ni zao la jamii, na ni kipengele muhimu sana cha utamaduni wa
jamii husika. Pili, lugha hutumiwa na jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake
na hasa kama chombo maalumu cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo isimu
jamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo
ndiyo mama wa lugha.
5.5.3. Isimu anthropolojia
– tawi hili la isimu hukijita katika kutafiti na kueleza historia ya na miundo
ya lugha ambazo bado hazijaandikwa.
5.5.4. Isimu kompyuta
– huchunguza matumizi ya kompyuta katika kuchakata na kuzalisha lugha ya
mwanadamu. Ni tawi ambalo kwa hakika si la muda mrefu na linatokana na
maendeleo ya sayansi na tekinolojia hasa baada ya uvumbuzi wa kifaa kama
kompyuta.
5.5.5. Isimu tumizi
– huchambua na kueleza matumizi ya nadharia mbali mbali za lugha na maelezo ya
kufundishia lugha.
5.6.
Ujuzi wa Lugha na Mjua Lugha
Swali la msingi
tunaloweza kujiuliza ni kuwa, “mjua lugha
ni nani?” na “kujua lugha ni nini?”
Katika hali ya kawaida imekuwa ni mazoea mtu kusema “mimi ninajua lugha” au
“hawa hawajui lugha”. Lakini je ni nini hasa kujua lugha? Majibu yake ni kama
yafuatayo:
i.
Kujua lugha ni uleuwezo wa kutabua na
kubainisha sauti pekee za lugha
ii.
Kujua lugha ni kujua namna sauti hizo
zinavyoungana
iii.
Kujua lugha ni kujua namna maneno
yanavyowezwa kuundwa na kugawanywa
iv.
Kujua lugha ni kujua namna maneno
yananyoungana kutengeneza tungo
v.
Kujua lugha ni kujua naana ya maneno na
visemo mbali mbali vya kugha husika
vi.
Kujua lugha ni kuweza kutumia lugha hiyo
katika muktadha wa mawasiliano
Kwa maelezo hayo
tunakuwa tumejibu swali la kuwa kujua lugha ni nini. Swali la mjua lugha ni
nani hapa linakua sitata tena kwani mtu anaye kuwa anasifa zote hizo hapo juu
tunasema huyu ni mjua lugha.
6.0.
Muundo wa Lugha
Hoja kuwa lugha ni
mfumo inamaanisha kuwa lugha inamuundo unaohusisha viambajengo mbali mbali.
Viaambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio
hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au
kama haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha. Viambajengo hivi,
hushughulikiwa na tanzu tofauti tofauti za isimu muundo. Tanzu hizi ni Fonetiki na fonolojia – ambazo hushughulikia sauti za lugha, mofolojia – ambayo hushughulikia maumbo
ya maneno na jinsi lugha inavyounda maneno yake, sintaksia – ambayo hushughulikia namna senteni zinavyoundwa na
kanuni zinazotawala uundwaji wake na mwisho ni semantiki – ambayo hushughulikia maana katika viwango vyote vya vya
lugha tulivyo vitaja. Kwa ujumla tanzu hizi zote zinahusiana kwa ukaribu,
zina shirikiana, na kukamilishana. Tazama mchoro ufuatao: